KUAPISHWA KWA BI ANNA ELISHA MGHWIRA
Rais wa jamhuri ya
muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amemuapisha aliyekuwa mgombea urais mwaka 2015 kupitia chama cha ACT wazalendo
Bi Anna Elisha Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro .
Bi Anna Elisha Mghwira amechukua nafasi iliyoachwa wazi na
Bw. Saidi Meck Sadiki aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo .
Akizungumza baada ya kumuapisha Rais Magufuli amemtaka Bibi
Anna Elisha Mghwira kwenda kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuondoa kero
zinazowakabili wananchi wa Kilimanjaro bila kujali itikadi za vyama vyao vya
siasa, dini, makabila na kanda wanazotoka.
"Mimi huwa siteui watu hivi hivi huwa naangalia uwezo
wa mtu na wewe nimekuchunguza na nimejiridhisha kuwa una uwezo wa kuwatumikia
wananchi nenda kachape kazi, kawaondolee kero wananchi wa Kilimanjaro, wapo
watu watakaokusema na wengine watakuonea wivu “amesema Dkt Magufuli, baada ya
kumuapisha katika Ikulu jijini Dar es Salaam.
Bi Mghwira amemshukuru Rais kwa kumuamini na kumteua kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na amemuahidi kuwa yupo tayari kwenda kufanya kazi
ya kuwatumikia wananchi na kujenga Taifa.
"Ninasema hii ni heshima kwa Taifa letu ni heshima kwa
umoja wa nchi yetu, ni heshima kwa siasa za umoja wa nchi yetu, kumekuwa na
minong'ono mingi sana kuwa Rais analeta nini, kuteua watu wanaitwa wapinzani,
mimi sio mpinzani wa maendeleo" amesema Bi Mghwira.
Bi Mghwira alikuwa mgombea pekee wa kike wakati wa kinyang'anyiro
cha urais mwaka 2015 na amekuwa mwenyekiti wa chama cha ACT wazalendo chama
ambacho ni kichanga Zaidi nchini Tanzania kilichoundwa mwaka 2014.
Mghwira mwenye umri wa miaka 56 anatoka mkoa wa Singida na Baba yake alikuwa diwani na kiongozi chama cha
Tanu ambacho kwa sasa kinajulikana kwa jina la CCM.

No comments: